Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu: Sakramenti ya Upendo
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican, leo Mama kanisa anasherehekea Fumbo la Ekaristi Takatifu kama inavyojulikana na wengi: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini. Kila Jumapili, waamini wanaadhimisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, iliyoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe, Siku ile ya Alhamisi kuu wakati wa Karamu ya Mwisho! Lakini, kila mwaka, Kanisa lina furaha kubwa ya kuadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu, kiini cha imani ya Kanisa kwa kumwabudu Kristo Yesu anayejisadaka na kujitoa kwa waja wake kama chakula na kinywaji cha wokovu! Kristo Yesu ni mkate na kinywaji kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele; ni sadaka ya Kristo mwenyewe kwa ajili ya binadamu! Mwana wa mtu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu ni Mwana Kondoo wa Pasaka, anayemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kumwongoza katika Nchi ya ahadi. Papa Leo XIV anasema, Kristo Yesu, katika maumbo ya Mkate na Divai, anaendelea kuwa kati pamoja na wafuasi wake, huku akiwakirimia nguvu ya kushinda kishawishi cha kukata na kujikatia tamaa, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa takatifu; Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kushiriki kikamilifu kwa ibada na heshima kuu wakati wa maandamano ya Ekaristi Takatifu, kwani hiki ni kielelezo makini cha uwepo angavu na endelevu wa Kristo katika maisha ya waja wake, Kristo anayeandamana na wafuasi wake, bega kwa bega! Huyu ni Kristo Yesu anayefanya hija ya imani pamoja na waja wake!
Ekaristi Takatifu inajenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe, linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kutoka kina cha mapendo yake Kristo ametupatia Ekaristi Takatifu ili mosi, tuiadhimishe, halafu tuile na tatu tuiabudu, katika Ekaristi uhai wetu unajipatia maana, unakua na kukomaa hatua kwa hatua na kufikia kipeo chake mbinguni. Sherehe hii ni ushuhuda wa imani yetu ya msingi kwamba Yesu yuko hai na anajitoa kwetu katika Mwili na Damu Yake. Ekaristi ni, Ukumbusho wa mateso, kifo, na ufufuko wa Kristo, Sadaka ya milele kwa ajili ya ukombozi wa dunia, Chakula cha uzima wa milele, Kielelezo cha umoja wa Kanisa. Tunapoabudu, kuadhimisha na kuila Ekaristi Takatifu tuombe neema ya kudumisha umoja na upendo wa Kiekaristia kwa kuishi mashauri ya Injili na kweli za imani yetu. Kristo anatuagiza leo tuoneshane upendo wa kiekaristia kwa kuwa wakarimu akisema ‘wapeni ninyi kula’.. Ni agizo la Kristo kwa Mitume anapoongeza mikate na samaki ni muujiza unaosimuliwa na Injili zote, Mt 14, Mk 6, Yn 6 na Lk 9 ukifungasha chembechembe zote za Ekaristi Tatakatifu.
UFAFANUZI: WAPENI NINYI KULA ni mwaliko wa kuleta hali njema baina yetu kiroho na kimwili kwa kusaidiana katika vipengele muhimu vya maisha na hivi kuunda jamii mpya ya haki, amani na salama. Wenye shida za kimwili na za kiroho, walio na huzuni, mawazo na waliokata tamaa hawana haja ya kwenda zao wakajinunulie, bali wapeni ninyi kula. Katika Injili, Yesu anawalisha maelfu, akidhihirisha kwamba huruma ya Mungu haina kikomo. Ndivyo alivyo katika Ekaristi – anajitoa bila kipimo kwa kila mmoja wetu. Baba Mtakatifu kupitia ujumbe wa kimataifa wa siku hii anasisitiza kwamba: “Ekaristi ni chanzo cha matumaini duniani – maana ni Yesu mwenyewe anayetufundisha kugawa, kusamehe, na kuishi kwa ajili ya wengine.” Katika dunia ya njaa – si ya chakula tu bali ya upendo, ya haki, na ya maana – Ekaristi inakuwa chakula cha matumaini. Ni mwito kwa kila Mkristo kuwa mkate unaovunjika kwa ajili ya wengine. Sekwensia ya Ekaristi inatukumbusha “..hula wema na wabaya, kwa bahati mbalimbali, kifo au uzima... basi mkate mkate mtakatifu, huwa sumu kwa wabaya.. dawa bora kwa wema, alleluia…” chunguza nafsi yako, usipokee sababu ya mazoea, majivuno, hofu ya macho ya watu au kujionesha kuwa unakomunika, hapo huwa hasara kubwa ya roho, ni kama chakula kizuri katika sahani chafu na tendo zima la chakula linageuka kuwa mashaka. Sherehe ya Ekaristi mwaka huu inafanyika katika mwangaza wa Jubilei ya Matumaini, ikisisitiza, Yesu yuko nasi – daima na kwa upendo usiokoma, Tumaini linashamiri pale tunapogawana kile tulicho nacho, Ekaristi hutufundisha kushukuru, kugawa, na kupenda, Katika Jubilei hii, tunaalikwa kuiona meza ya Ekaristi si tu kama ibada, bali pia kama shule ya huruma, haki na mshikamano.
Sherehe za leo zitapungua uzito ndani mwetu iwapo tunampokea Yesu wa Ekaristi pasi na mapatano na wenzetu.. huenda tunasalimiana na kuzungumza sababu ya utu uzima tu lakini hatuna nia ya dhati... Tunadhihirisha kifungo cha mapendo na umoja wa kiekaristia kwa maelewano na watu wangapi? na hao wengine Je? changamoto ni nini? katika mazingira haya, amini ndugu yangu Ekaristi inakuwa kama mkate tu kutoka bekari... Kristo anapoagiza ‘wapeni ninyi kula’ anatamani tuwekeane hali njema ya amani, umoja na msamaha. Katika hotuba zake, Papa Leo XIV amekuwa akihimiza waamini, Waishi Ekaristi kila siku, si tu kuipokea bali kuwa kielelezo cha upendo wa Kristo duniani. Kanisa liwe la ekaristi: limkaribishe kila mtu, libebe mzigo wa wengine, na ligawane mali kwa usawa. Maaskofu, mapadre, na waamini wa kawaida wawe mashahidi wa tumaini kwa njia ya ekaristi inayoishi katika matendo. “Yesu si chakula cha roho tu, bali ni mfano hai wa dunia mpya yenye matumaini, mshikamano, na amani.” Halafu leo tuwakumbuke wagonjwa wasioweza kukomunika, Yesu wa Ekaristi awape kitulizo na faraja katika mahangaiko yao, waunganishe mateso yao na yale ya Kristo Msalabani. Nasi tujibidiishe katika mwenendo mwema, tukijitahidi kuepa dhambi na kuiishi Ekaristi Takatifu tupate kugeuzwa nayo, Kristo awe jawabu pekee la maisha yetu, Kiongozi wetu, awe faraja yetu, tuepukane na hofu tukawe vyombo vyake na hivi kuzaa matunda mema… amina. Tunaalikwa, Kupokea Ekaristi kwa heshima, Kuishi Ekaristi katika kushukuru, kusamehe, na kuto Kuwa Ekaristi kwa wengine – katika huduma, upendo, na hak “Katika Ekaristi tunamwona Yesu anayetoa kila kitu, nasi tuwe tayari kujitoa kama mkate uliovunjika kwa ajili ya dunia yenye njaa na kiu ya Mungu.” Ee Yesu Ekaristi, tukufurahie katika sakramenti hii takatifu. Tufanye tuwe watu wa matumaini, wenye kugawa na kupenda, ili dunia ifurahi katika uwepo wako wa milele. Amina.