Ujumbe Wa Papa Leo XIV Jubilei ya Miaka 500 ya Kanisa la Mennonite
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utengano kati ya Wakristo hupingana wazi na mapenzi ya Kristo Yesu na ni kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu la kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mtakatifu Yohane Paulo II alitaka kuona kwamba, Kanisa Katoliki linaendeleza majadiliano ya kiekumene na Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali, ili siku moja wote wawe wamoja chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mkuu. Kwa upande wake, Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma. Anasema uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.
Harakati za Anabaptisti zilianza huko Zurich kunako mwaka 1525 na kuenea haraka sana kama “moto wa mabua.” Hata hivyo, Wanabaptisti walidharauliwa, waliteswa, walinyang'anywa mali zao na kufukuzwa na Serikali na Kanisa. Miaka 500 baadaye, Waanabaptisti kutoka sehemu mbalimbali za dunia, katika maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana, tarehe 29 Mei 2025, wamekutana mjini Zurich nchini Uswisi, kuadhimisha Jubilei ya Miaka 500 ya Harakati za Anabaptisti, tukio ambalo limeandaliwa na Mkutano wa Ulimwengu wa Mennonite, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “ujasiri wa kupenda.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Harakati za Anabaptisti, anakazia zaidi amani kutoka kwa Kristo Mfufuka: Rej Yn 20:19 inayowakirimia Mitume ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa bila woga, huku wakiwa na mwanga mpya wa mwili wa utukufu wa Kristo Yesu uliokuwa bado na makovu ya mateso yake. Kwa kupokea zawadi hii ya amani, wanakuwa wazi kupokea karama na mapaji ya Roho Mtakatifu yanayopyaisha imani na maisha ya Kikristo, mambo yaliyotendwa na Harakati za Anabaptisti.
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Harakati za Anabaptisti yananogeshwa na kauli mbiu “Ujasiri wa kupenda” huu ni mwaliko kwa Wakatoliki na waamini wa Kanisa la Mennonite kujizatiti zaidi katika kuimwilisha Amri ya Upendo katika uhalisia wa maisha yao, ili kukuza na kudumisha umoja wa Wakristo, tayari kuwahudumia jirani zao. Huu ni wito kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu na wakarimu, kwa kutafakari makovu ya historia ya Makanisa haya mawili; ni historia inayogubikwa na madonda yaliyosababisha mahusiano na mafungamano tenge, hali ambayo bado inaendelea kujionesha hata leo hii katika Ulimwengu mamboleo. Kumbe kuna haja ya kutakasa kummbukumbu na hatimaye kuanza upya kusoma upya historia ya maisha na utume wao, tayari kujikita katika mchakato wa uponyaji wa madonda yaliyopita ili, ili kupyaisha maisha yao ya mbeleni kwa njia ya ujasiri wa kupenda. Huu ni mwaliko kwa Makanisa haya kuendelea kujikita katika majadiliano ya kitaalimungu ambayo yatazaa matunda yanayodumu. Rej Yn 15:16. Baba Mtakatifu Leo XIV anakiri kwamba, hili si jambo dogo, lakini ni muhimu kwa Wakristo kujikita katika Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani zao Re. Mt 22: 34-40; na kuendelea kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa umoja, ili wote wawe na umoja, ili ulimwengu upate kusadiki. Rej Yn 17:21. Kama anavyosema Mtakatifu Augustino matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV yanafumbatwa katika huruma yao na utekelezaji wake. Anapenda kuwaalika waamini wa Kanisa la Mennonite kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, kama kielelezo cha ushuhuda wa Kristo Yesu Mfalme wa Amani, ili kwa pamoja waweze kujenga utamaduni wa upendo na watu kukutana. Mwishoni, Papa Leo XIV amewahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala, ili kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano baina ya Makanisa haya mawili, mwishoni, amewapatia baraka zake za kitume zinazobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka.