Baba Mtakatifu Leo XIV Shukrani Kwa Ushiriki wa Watu wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste yanahitimisha pia Kipindi cha Pasaka na hivyo Sala ya Malkia wa Mbingu, kwa maadhimisho haya inasitishwa. Baba Mtakatifu Leo XIV, kabla ya kuhitimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya Sherehe ya Pentekoste, amewashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema walioshiriki katika maadhimisho haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Amewashukuru Makardinali, Maaskofu pamoja na wawakilishi wa vyama, mashirika ya kitume na jumuiya mpya walioshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Jubilei yao ambayo imefikia hatima yake kwa Ibada ya Misa Misa Takatifu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, kwa njia maadhimisho ya Jubilei hii, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu watakuwa wamepyaishwa, changamoto na mwaliko kwa kila mshiriki ni kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kutoka kwa Kristo Yesu.
Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbuka wanafunzi wanaokaribia kufunga shule na hivyo kuanza likizo ya kipindi cha kiangazi. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwasalimia wanafunzi na walimu wao wanaojiandaa kwa mitihani yao ya mwisho wa Mwaka. Mwishoni, kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa amewaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu zawadi ya amani katika nyoyo zao, kwani ni katika moyo uliosheheni amani tu ndio unaoweza kueneza amani katika familia, katika jamii na katika mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Roho wa Kristo Yesu Mfufuka afungue njia za upatanisho popote palipo na vita; aziangazie Serikali na azipe ujasiri wa kufanya ishara za majadiliano yanayoonekana.