Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia zaidi kuhusu: Dhamana na Kazi ya Roho Mtakatifu kama: Chemchemi ya umoja na ushirika Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia zaidi kuhusu: Dhamana na Kazi ya Roho Mtakatifu kama: Chemchemi ya umoja na ushirika  (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV: Mahubiri Sherehe ya Pentekoste 2025: Kazi za Roho Mtakatifu

Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia zaidi kuhusu: Dhamana na Kazi ya Roho Mtakatifu kama: Chemchemi ya umoja na ushirika; anafungua mipaka kutoka katika undani wa maisha ya waamini; anawakirimia waamini njia mpya ya kutazama mambo na kuishi; Roho Mtakatifu anafungua mipaka ya mahusiano na mafungamano ya kijamii; Anakuza na kukomaza matunda ya Roho Mtakatifu na hatimaye, anafungua mipaka kati ya watu wa Mataifa! Umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana aliyenena kwa vinywa vya manabii. Kanisa, ushirika hai katika imani ya Mitume ambayo linaiendeleza, ni mahali muafaka kabisa pa kumjua Roho Mtakatifu: Katika Maandiko Matakatifu ambayo ameyavuvia; Katika Mapokeo ambayo Mababa wa Kanisa siku zote ndio Mashuhuda wake halisi, Katika Mamlaka fundishi ndani ya Kanisa “Magisterium”; katika Liturujia ya Sakramenti za Kanisa kwa maneno na alama zake ambamo Roho Mtakatifu anawaingiza waamini katika ushirika na Kristo Yesu, Katika sala ambako anawaombea; katika karama na huduma zinazolijenga Kanisa; Katika Ishara na maisha ya kitume na kimisionari; Katika ushuhuda wa watakatifu, ambamo anadhihirisha utakatifu wake na kuendeleza kazi ya ukombozi. Rej. KKK 683-730. Sherehe ya Pentekoste ni siku ya hamsini, hitimisho la Pasaka ya Bwana, Roho Mtakatifu anawashukia Mitume na hivyo kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu; kutoka katika utimilifu wake Kristo Yesu, Bwana anammimina Roho kwa wingi. Hii ni siku ambayo Fumbo la Utatu Mtakatifu linafunuliwa kwa ukamilifu. Toka siku hiyo, ufalme uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu uko wazi kwa ajili ya wale wanaomwamini na kumsadiki, katika hali ya unyenyekevu na imani wanashiriki ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni paji la Mungu na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamini wanaweza kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu ambayo: ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Rej. KKK 731-747.

Dhamana na Kazi ya Roho Mtakatifu: Umoja na upendo
Dhamana na Kazi ya Roho Mtakatifu: Umoja na upendo   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, Dominika tarehe 8 Juni 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican sanjari na Jubilei ya Vyama, Mashirika na Jumuiya Mpya, matunda na kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho haya yamenogeshwa na kauli mbiu “Uinjilishaji na Malezi Katika Mwanga wa Matumaini ya Kikristo. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia zaidi kuhusu: Dhamana na Kazi ya Roho Mtakatifu kama: Chemchemi ya umoja na ushirika; anafungua mipaka kutoka katika undani wa maisha ya waamini; anawakirimia waamini njia mpya ya kutazama mambo na kuishi; Roho Mtakatifu anafungua mipaka ya mahusiano na mafungamano ya kijamii; Anakuza na kukomaza matunda ya Roho Mtakatifu na hatimaye, anafungua mipaka kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu baada ya mateso, kifo, ufufuko na kutukuzwa kwa kupaa kwake mbinguni, aliwashushia Mitume na wafuasi wake Roho Mtakatifu, akawakirimia mapaji yake na hivyo kuanza kuzungumza kwa lugha nyingine. Rej. Mdo 2: 1-11. Mitume waliokuwa wamejifungia kwa hofu baada ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, wakajaliwa akili ya roho, ili kutafsiri matukio mbalimbali ya maisha kwa mwanga wa uwepo angavu wa Kristo Mfufuka.

Roho Mtakatifu anafungua mipaka na kuimarisha mafungamano ya kijamii
Roho Mtakatifu anafungua mipaka na kuimarisha mafungamano ya kijamii   (@VATICAN MEDIA)

Roho Mtakatifu anawakirimia nguvu ya kushinda woga na hofu; anavunjilia mbali minyororo ya ndani, anaganga na kutibu madonda na hivyo kuwakirimia ujasiri wa kutoka ili kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu. Roho Mtakatifu alifungua mipaka, ili Mitume na wafuasi wa Kristo Yesu waweze kuelewa, anavunjilia mbali mkanganyiko wa lugha uliojitokeza wakati wa ujenzi wa Mnara wa Babeli, kielelezo cha kiburi na jeuri ya mwanadamu. Mnara wa Babeli ni kiashiria cha kuchanganyikiwa na hali ya kukata tamaa, mwaliko wa kuambata lugha inayojenga umoja na ushirika; lugha ya upendo, ukaribu na huduma; lugha inayowafungulia watu mipaka na kwamba, hii ni dhamana ya Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anawafungulia watu mipaka, anavunjilia mbali kuta za utengano kati ya makundi ya watu. Roho Mtakatifu anafungua mipaka kutoka katika undani wa watu wenyewe na hivyo kuwakirimia zawadi ya upendo katika maisha.

Ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu
Ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo IV anasema, uwepo angavu wa Kristo Mfufuka unayeyusha ugumu wa nyoyo za waamini, unavunjilia mbali tabia ya uchoyo na ubinafsi; hali ya kujifungia wenyewe, ili hatimaye, waamini waweze kujenga mtandao wa umoja na mshikamano. Roho Mtakatifu anawakirimia waamini njia mpya ya kutazama mambo na kuishi, anawaongoza katika njia ya kukutana na Kristo Mfufuka, huku akiwafundisha kukita maisha yao katika furaha ya Injili, huku wakiendelea kukaa katika pendo lake, pamoja na kulishika Neno lake, linalowaletea mabadiliko katika maisha na hivyo kuwawezesha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya ukarimu. Roho Mtakatifu anawawezesha kufungua mahusiano na mafungamano ya kijamii na hivyo kuwakirimia upendo unaomwezesha Mungu Baba wa milele kufanya makao kati ya ona hivyo kuwawezesha kung’oa ndani mwao ule ukaidi, woga na wasiwasi wa tofauti msingi katika maisha na hivyo kulea na kukomaza hisia ndani ya waamini. Roho Mtakatifu anaganga na kuponya maamuzi mbele, ugandamizaji na unyonyaji, vita na tabia ya kutaka kulipiza kisasi pamoja na ongezeko kubwa la mauaji ya wanawake.

Uwepo angavu wa Kristo Mfufuka unayeyusha ugumu wa nyoyo
Uwepo angavu wa Kristo Mfufuka unayeyusha ugumu wa nyoyo   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Roho Mtakatifu anawajalia waamini kukuza na kukomaza matunda ya Roho Mtakatifu, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kweli na bora zaidi: “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.” Gal 5: 22-26. Ni katika muktadha huu, Roho Mtakatifu anapanua mahusiano na mafungamano ya waamini na hivyo kuwawezesha kujikita katika furaha ya udugu wa kibinadamu. Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni sehemu ya Kanisa la Kristo Mfufuka na Mitume wa Pentekoste, ikiwa kama watasimama kidete kujenga umoja na ushirika; kwa kuzama zaidi katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; ikiwa kama watapokeana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi; na ikiwa kama Kanisa watageuka na kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo na ukarimu kwa wote.

Roho Mtakatifu anawajalia waamini kukuza na kukomaza matunda ya Roho
Roho Mtakatifu anawajalia waamini kukuza na kukomaza matunda ya Roho   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Roho Mtakatifu anafungua mipaka hata kati ya watu na hivyo kuvunjilia mbali ule mkanganyo wa lugha uliojitokeza wakati wa ujenzi wa Mnara wa Babeli, kwa kuishi katika umoja, upendo, amani na utulivu, matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu. Ni Roho Mtakatifu anayewaunganisha na hivyo kuwakirimia uwezo wa kuona ile sura ya jirani zao kama amana na utajiri na wala si adui wa kufyekelea mbali. Kumbe, kama ndugu wanaweza kuchota amana na utajiri huu, tayari kutembea kwa pamoja katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kuvunjilia mbali kuta za utengano, chuki na uhasama kwa sababu “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” Yn 14:26. Jambo la msingi kwa waamini kukumbuka ni ile Amri ya upendo, kiini na utimilifu wa maisha yote. Penye upendo hakuna nafasi ya maamuzi mbele, wala utengano kwa kisingizio cha usalama na matokezo yake ni kuibuka kwa wanasiasa wanaotaka kujimwambafai kwa utaifa usiokuwa na tija wala mashiko. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste mwaka 2023 aliona kwamba, kuna mafarakano na migawanyiko mingi duniani, na watu wengi wanajikuta wakiwa wametenganishwa na hatimaye, kupigwa ganzi ya kutojali na hivyo kukandamizwa na upweke hasi. Bado dunia hii inatikiswa na vita, ishara mbaya sana.

Tunda la Roho ni Upendo, furaha, amani, uvumilivu na utu wema
Tunda la Roho ni Upendo, furaha, amani, uvumilivu na utu wema   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Roho Mtakatifu, Roho wa upendo na amani, apate kufungua mipaka, kubomoa kuta, kufutilia mbali chuki na uhasama na hivyo kuwasaidia watu wa Mungu kuishi kama watoto wa Baba mmoja aliye mbinguni. Sherehe ya Pentekoste inalipyaisha Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Upepo mkali wa Roho Mtakatifu uwashukie na kukaa ndani ya waamini; ufungue mipaka ya nyoyo zao, uwakirimie neema na baraka za kukutana na Mwenyezi Mungu; Roho Mtakatifu apanue upeo wa upendo wao na aunge mkono juhudi za waamini za kujenga ulimwengu ambamo amani inatawala. Hatimaye, Bikira Maria, Mama wa Pentekoste aliyetembelewa na Roho Mtakatifu, akajazwa neema, awasindikize na kuwaombea waamini wote.

Papa Leo XIV Pentekostre 2025

 

08 Juni 2025, 15:21