Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumanne tarehe 10 Juni 2025 amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa Vatican katika nchi mbalimbali na katika Mashirika ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumanne tarehe 10 Juni 2025 amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa Vatican katika nchi mbalimbali na katika Mashirika ya Kimataifa.   (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV: Mabalozi wa Vatican Kielelezo Cha Diplomasia ya Kanisa Katoliki

Papa Leo XIV: Mabalozi ni kielelezo cha Kanisa Katoliki, Diplomasia ya Vatican; Utume wao sanjari na mahusiano na mafungamano kati ya Mabalozi wa Vatican na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika huduma ya upendo; ushuhuda; utii na ushirika katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Wao ni wamisionari na kwamba, kuna Mapapa ambao wamekuwa wawakilishi wa Vatican sehemu mbalimbali za dunia, leo hii ni mfano bora wa kuigwa katika utakatifu wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Vatican kwenye nchi na mashirika mbalimbali ya Kimataifa wanapaswa kutambua kwamba: Wao ni watu wa Mungu, wanaopaswa kuheshimu na kutekeleza Amri za Mungu na kuishi kadiri anavyotaka Mungu, kiasi hata cha kukubali kupokea mateso, shida na changamoto mbalimbali za kiimani. Balozi wa Vatican ni mtu anayeongozwa kwa Neno la Mungu, ili kuweza kufikiri, kuamua na kutenda; daima akijikabidhi na kujiaminisha katika ulinzi na tunza ya Mungu. Ni mtu asiyekubali kiurahisi kumezwa na malimwengu. Sifa za mtu wa Mungu ni pamoja na: haki, upendo, huruma, ibada na msamaha! Pale wanaposhindwa kujitambua kwamba, ni watu wa Mungu wanakuwa ni chanzo cha kuanguka kwao wenyewe pamoja na kusababisha madhara kwa watu wengine. Mabalozi wa Vatican sehemu mbalimbali za dunia ni madaraja, mashuhuda na vyombo vya majadiliano kati ya watu wa Mataifa! Wanapaswa kutambua kwamba, wao ni madaraja muhimu sana kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia; Jamii za watu pamoja na Jumuiya ya Kimataifa na wanapaswa kugundua kwamba Kanisa ni kama “Hospitali kwenye uwanja wa mapambano”, ili kuganga na kuponya majeraha ya watu kutokana na sababu mbalimbali za maisha. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumanne tarehe 10 Juni 2025 amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa Vatican katika nchi mbalimbali na katika Mashirika ya Kimataifa. Mabalozi hawa, Jumatatu tarehe 9 Juni 2025 wameshiriki pia katika Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, ambayo inaadhimishwa, Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste na kwa mwaka huu ni tarehe 9 Juni 2025. Maadhimisho ya Mwaka huu, yanabeba uzito wa pekee kwani ni sehemu pia ya maadhimisho ya Jubilei ya Vatican: “Kiti kitakatifu” “Holy See.”

Askofu mkuu Novatus Rugambwa afya yake ikiendelea kuimarika.
Askofu mkuu Novatus Rugambwa afya yake ikiendelea kuimarika.

Maadhimisho yalianza kwa wafanyakazi wa Vatican kushiriki katika Ibada ya Maungamo, tafakari iliyoongozwa na Sr. Maria Gloria Riva, wa Shirika la Watawa Wanaoabudu Daima Ekaristi Takatifu, tafakari ambayo imehudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Leo XIV, ambaye baadaye ameongoza Maandamano ya wanahija kuelekea Mlango Mtakatifu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, huku akiwa amebeba Msalaba na hatimaye, akaongoza pia Ibada ya Misa Takatifu. Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake, amejikita zaidi katika kufafanua kwamba: Mabalozi ni kielelezo cha Kanisa Katoliki, Diplomasia ya Vatican; Utume wao sanjari na mahusiano na mafungamano kati ya Mabalozi wa Vatican na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika huduma ya upendo; ushuhuda; utii na ushirika katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Wao ni wamisionari na kwamba, kuna Mapapa ambao wamekuwa wawakilishi wa Vatican sehemu mbalimbali za dunia, leo hii ni mfano bora wa kuigwa katika utakatifu wao.. Mabalozi wanatoa huduma ya uteuzi wa Maaskofu, huduma ambayo haina mbadala. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha Mabalozi hawa kwamba, wao ni kielelezo cha Kanisa Katoliki na wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbalimbali za dunia, kielelezo cha ujenzi wa umoja na ushirika, kwa kuungana na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. katika mchakato wa kidiplomasia ya Vatican na uhusiano wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa, Vatican kwa namna ya pekee inakazia: Mosi, umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Jambo la pili, ni uhamasishaji wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga na kuimarisha: haki, umoja na udugu wa kibinadamu ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Vatican inakazia: ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutatua migogoro ya kivita, mipasuko, kinzani na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia!

Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa
Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa   (@Vatican Media)

Lengo la diplomasia ya Vatican ni kukuza na kudumisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Katika sehemu hii, Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii na hasa zaidi sauti ya watu wasiokuwa na sauti! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu wote bila ubaguzi. Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata maendeleo ya kweli na endelevu, basi binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani! Kanisa linapenda kudumisha mchakato wa haki, amani, utulivu na maridhiano kwa kuzimisha moto wa machafuko, kinzani na vita kwa maji ya baraka, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa ufupi ni Diplomasia inayokita mizizi yake katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, haki na amani kati ya watu wa Mataifa. Mabalozi ni wasaidizi wa karibu sana wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kuandaa: Nyaraka, tafakari na kwamba, mtandao wa mabalozi na wawakilishi wa Vatican unatenda mintarafu shughuli za kichungaji na imani inayowasukuma kutenda na hivyo kumwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kushiriki katika maisha na utume wa watu wa Mungu wanaowawakilisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kiwete aliyeponywa na Mtakatifu Petro na Yohane pale hekaluni, ni muhtasari wa maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, huu ni ushuhuda kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufufka kutoka wafu ni mzima, chemchemi ya matumaini kwa watu waliokata tamaa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii; wao wanatenda kwa jina la Kristo Mfufuka.

Kardinali Pietro Parolin, akizungumza na Papa Leo XIV
Kardinali Pietro Parolin, akizungumza na Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Mabalozi wa Vatican ni wahudumu wanaohamasishwa kuwatazama watu wa Mungu, tayari kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano; huduma inayotekelezwa kwa unyenyekevu; na kutendwa kwa jina la Kristo Yesu. Khalifa wa Mtakatifu Petro hana majibu ya matatizo, changamoto na fursa zote zinazojitokeza katika maisha ya watu wa Mungu, lakini wanatenda kwa nguvu ya Kristo Mfufuka. Watambue kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo, huku wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, walengwa wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu ni maskini. Upendo ni kielelezo cha imani na kwamba, wao ni wahudumu wa waathirika wa vita, machafuko, ukosefu wa haki msingi pamoja na dhana ya maendeleo potofu yanayodanganya watu. Mabalozi hawa wanafanya kazi katika kivuli cha Khalifa wa Mtakatifu Petro, wanatenda kazi kwa kushirikiana na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, wametumwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, utume wanaopaswa kuutekeleza kwa kuendelea kujikita katika utii, umoja na ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kwa pamoja waweze kushiriki katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, daima wakikuza na kudumisha umoja na Maaskofu mahalia. Mabalozi na Wawakilishi wa Vatican wanatumwa kuwabariki watu wa Mungu. Mabalozi watambue kwamba, wao ni wamisionari wameitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa umoja na ushirika, huduma kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujenga mahusiano na mafungamano bora na wakuu wa Serikali na nchi husika, ili kuendeleza ushirikiano, daima wanachangamotishwa kujibidiisha kutafuta utakatifu wa maisha, kwani hata katika huduma hii ya diplomasia ya Kanisa wako Mababa watakatifu Yohane XXIII na Paulo VI ambao wamejipambanua kwa utakatifu wa maisha yao. Dhamana na utume wa Mtakatifu Petro ni kuwaimarisha ndugu zake katika imani, lakini Mabalozi na wawakilishi wa Vatican wanapaswa kwanza kabisa kuimarishiwa imani yao, ili hatimaye waweze kuwa ni wajumbe wa tunu hizi msingi, sehemu mbalimbali za dunia. Kwa kupitia kwenye Lango kuu la Huruma ya Mungu, Kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, wanaitwa sasa kuwa ni mashuhuda jasiri wa Kristo Yesu, chemchemi ya matumaini kwa waja wake.

Pete ya Kiaskofu zawadi kutoka kwa Papa Leo XIV kwa Mabalozi wa Vatican
Pete ya Kiaskofu zawadi kutoka kwa Papa Leo XIV kwa Mabalozi wa Vatican

Kwa upande wake Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amemwelezea Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, mkutano huu ulikuwa unahudhuriwa na Mabalozi 98, Wawakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Kimataifa 5 pamoja na Wawakilishi kadhaa wa Vatican wenye majukumu maalum. Baadhi hao wamepata hudhuru kutokana utekelezaji wa majukumu mbalimbali. Lakini katika mkutano huu na Baba Mtakatifu amehudhuria pia Askofu mkuu Novatus Rugambwa, ambaye kwa sasa anakabiliwa na changamoto ya afya, na wamemwombea uponaji wa haraka ili aweze tena kurejea kwenye shughuli na majukumu yake. Wanamshukuru Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuwashirikisha katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo; Kwa kukutana na kuzungumza nao pamoja na kupata nao chakula, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na ushirika. Mabalozi na wawakilishi wa Vatican sehemu mbalimbali za dunia ni vyombo na mashuhuda wasiokuwa na mbadala.

Balozi wa Vatican ni mtu wa Mungu na Kanisa
Balozi wa Vatican ni mtu wa Mungu na Kanisa   (@Vatican Media)

Itakumbukwa kwamba, Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Juni 2019 alikutana na Mabalozi wa Vatican kutoka sehemu mbalimbali za dunia na akatumia fursa hii kuwakumbusha Kanuni 10 wanazopaswa kuzingatia katika maisha na utume wao kama Mabalozi na Wawakilishi wa Vatican sehemu mbalimbali za dunia! Mosi, watambue kwamba, wao ni watu wa Mungu, wanaopaswa kuheshimu na kutekeleza Amri za Mungu na kuishi kadiri anavyotaka Mungu, kiasi hata cha kukubali kupokea mateso, shida na changamoto mbalimbali za kiimani. Anasema, Balozi wa Vatican ni mtu anayeongozwa kwa Neno la Mungu, ili kuweza kufikiri, kuamua na kutenda; daima akijikabidhi na kujiaminisha katika ulinzi na tunza ya Mungu. Ni mtu asiyekubali kiurahisi kumezwa na malimwengu. Sifa za mtu wa Mungu ni pamoja na: haki, upendo, huruma, ibada na msamaha! Pale wanaposhindwa kujitambua kwamba, ni watu wa Mungu wanakuwa ni chanzo cha kuanguka kwao wenyewe pamoja na kusababisha madhara kwa watu wengine. Pili, Balozi wa Vatican ni mtu wa Kanisa kwani anamwakilisha Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa. Anapaswa kuwaheshimu, kuwalinda na kuwaendeleza wale wote anaokutana nao katika maisha na utume wake, kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni kwa ajili ya huduma inayofumbatwa katika unyenyekevu. Ni watu wanaopaswa kushuhudia fadhila za kibaba na kichungaji. Makatibu na Washauri wa Balozi za Vatican ni viongozi ambao wako kwenye mafunzo, ili kwamba, siku moja waweze hata wao kuwa ni Mabalozi kadiri ya mpango wa Mungu. Mabalozi wa Vatican wawe ni watu wa kiasi, wakazie mambo msingi kwa kutambua kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma kwa wote!

Balozi wa Vatican ni mpatanisho na mjenzi wa umoja na mshikamano
Balozi wa Vatican ni mpatanisho na mjenzi wa umoja na mshikamano   (@VATICAN MEDIA)

Wawe wanyenyekevu wanapotambulisha Uso wa Kanisa, Mafundisho na Msimamo wa Kanisa kwa kuweka kando mambo binafsi, tayari kulinda na kulitetea Kanisa dhidi ya maadui wa ndani na wa nje! Mabalozi wajenge na kudumisha uhusiano na mafungamano na Maaskofu mahalia, Wakleri, Watawa na Waamini walei kwa kuwasindikiza katika utekelezaji wa maisha na utume wa Kanisa mahalia, yote haya yawe ni kwa ajili ya wokovu wa roho za watu! Sherehe kuu za Kanisa yaani: Noeli na Pasaka ni nyakati za kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na watu wa Mungu wanaounda familia yake. Tatu, Balozi wa Vatican ni mtu mwenye ari na mwamko wa kitume, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa mwanga wa Kristo Mfufuka. Ni kiongozi anayepandikiza mbegu ya imani, matumaini na mapendo na matunda yake ni sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu aliyemkomboa binadamu kwa kumwaga Damu yake Azizi pale Msalabani! Wajivunie kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, bila woga wala makunyanzi. Ari na mwamko wa kitume, unawalinda viongozi wa Kanisa ili wasitumbukie kwenye “saratani ya mawazo ya udanganyifu.” Nne, Balozi wa Vatican ni mpatanishi, ni mjenzi wa umoja, chachu ya majadiliano na maridhiano kati ya watu; ni mtu asiyekuwa na upendeleo na anayesimamia malengo, mwamuzi mwenye haki, mkweli na muwazi, anayepania kudumisha misingi ya haki na amani bila ya kuruhusu kutumiwa kinyume chake. Ni chombo cha mawasiliano na huduma kwa Maaskofu mahalia na watu wa Mungu katika ujumla wao. Ni kiongozi mwenye madaraka yanayolenga kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu na ushauri. Balozi wa Vatican anapaswa kujenga utamaduni wa kukutana na watu, ili kuimarisha umoja na maridhiano, kama mwakilishi wa sura ya Kanisa la Kiulimwengu mbele ya Makanisa mahalia na Serikali zao!

Balozi wa Vatican ni Mwakilishi wa Baba Mtakatifu
Balozi wa Vatican ni Mwakilishi wa Baba Mtakatifu   (@VATICAN MEDIA)

Tano, Balozi wa Vatican ni mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na anatenda kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na anatekeleza malengo yake kwa ajili Kanisa na viongozi wa Serikali. Ni mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, Ubalozi wa Vatican unapaswa kueleweka kuwa ni “Nyumba ya Papa.” Ni watu ambao wanapaswa kuondokana na unafiki kwani wao ni madaraja yanayomuunganisha Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na wanawanchi wanaowahudumia, kumbe ni wawakilishi wa Baba Mtakatifu. Dhamana na utume huu unahitaji: uwepo, uwezo wa kusoma alama za nyakati, unyenyekevu, weledi pamoja na uwezo wa kuwasiliana na kujadiliana na kwamba wao daima ni wasafiri. Balozi awe na uhusiano wa karibu na familia ya Mungu anayoihudumia, bila kusahau kujenga mahusiano mema na mafungamano na wanadiplomasia pamoja na viongozi wa Serikali. Awe na ari, bidii na moyo wa kutembelea Jumuiya zile ambazo hazitapata hata siku moja nafasi ya kutembelewa na Papa, kama kielelezo cha uwepo wa karibu wa Kristo na Kanisa lake. Wawe na ujasiri wa kwenda pembezoni mwa vipaumbele vya mwanadamu. Wawe ni mashuhuda wa Kristo Yesu katika maisha yao kwa kukazia ukweli na neema ya kushiriki amana na utajiri unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Mabalozi wa Vatican wanapaswa kujiendeleza na kujipyaisha kila wakati pamoja na kutoa taarifa kwa Papa kuhusu yale yanayoendelea kujiri katika uwakilishi wao. Wawe na ufahamu mkubwa wa tamaduni, mila, desturi na lugha ya watu mahalia; kwa kuwa wazi kwa wote. Wajiepushe kujiunga na makundi ya mitandao inayoonesha kinzani na ukakasi kwa Sekretarieti kuu na Kanisa la Roma.

Balozi wa Vatican ni chombo cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Balozi wa Vatican ni chombo cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi   (@Vatican Media)

Sita, Balozi wa Vatican ni mtu anayechakarika usiku na mchana ili kufanikisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila “kuzenguliwa” na ugumu wa mawazo, kiroho na kiutu wala kutekeleza mambo yake kwa “mwendo wa kinyonga.” Huyu ni kiongozi anayehamasishwa kutafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima akiwa mwaminifu kwa dhamana na utume wake. Ni mtu anayeweza kusoma alama za nyakati, tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika hali ya utulivu na amani ya ndani. Watambue kwamba, wao ni Maaskofu na wachungaji, licha ya kuishi hapa duniani, lakini wakumbuke kwamba wao si wa ulimwengu huu, wawe na hekima kama nyoka na wapole kama njiwa. Kama wafuasi waaminifu wa Kristo Yesu, wajitahidi kuiga mifano ya Mitume na wafuasi wa kwanza wa Yesu, waliovutwa na hatimaye kuambatana na Kristo Yesu katika maisha yao! Saba, Balozi wa Vatican ni mtii anayetekeleza dhamana hii kwa uhuru wa ndani na kwamba, utii kwa Injili ni utimilifu wa utii wote. Utii wa kwanza unafumbatwa katika wito unaomwajibisha mtu kumfuasa Kristo Yesu, kwa kumtii Mungu zaidi, Kanisa na viongozi wake wakuu, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Utii ni dira katika mchakato wa kufikiri, kuamua na kutenda kwa hekima na unyenyekevu mkuu. Utii unakita mizizi yake katika: busara na upendo kwa Mungu na jirani. Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utii wa Kristo Yesu kwa Baba yake wa mbinguni. Mabalozi wa Vatican wawe mstari wa mbele kuonesha ushuhuda wa utii “Medice, cura te ipsum.” Nane, Balozi wa Vatican ni mtu wa sala anayetoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Kristo Yesu kama amana na utajiri anaopaswa kuutangaza, kuushuhudia na kuuwakilisha. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kristo Yesu kamwe hawezi kumtupa mtu anayemkimbilia na kumwambata. Wajenge utamaduni na mazoea ya kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu kwa njia ya sala, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni wahudumu waaminifu wa Neno la Mungu.

Balozi ni mtu anayetoa kipaumbele cha pekee kwa sala
Balozi ni mtu anayetoa kipaumbele cha pekee kwa sala   (@VATICAN MEDIA)

Tisa, Balozi wa Vatican ni mtu mwenye upendo tendaji unaomwilisha sala katika matendo ya huruma! Ni mtu anayethubutu kugeuza Fumbo la Ekaristi Takatifu na kuwa ni chemchemi ya Injili ya upendo kwa maskini, kama kielelezo cha imani tendaji. Ni kiongozi anayepaswa kujihusisha kikamilifu na shida pamoja na mahangaiko ya watu hususan katika masuala: ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya binadamu: kiroho na kimwili. Balozi wa Vatican atoe kipaumbele cha pekee kwa huduma ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama kielelezo makini cha utume na uwepo wake kama Baba na Mchungaji. Huu ni upendo unaomwilishwa katika sadaka na majitoleo; ili kusimamia haki na amani. Wawe makini ili wasipokee zawadi zitakazokwamisha uhuru wao na kuwatumbukiza katika utumwa. Kumi, Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Balozi wa Vatican anapaswa kuwa mnyenyekevu na mpole wa moyo kama alivyo Kristo Yesu. Kamwe asitake kupendwa, kutukuzwa, kuheshimiwa, kushangiliwa na kupewa upendeleo. Lakini badala yake, wakubali wanaponyenyekeshwa, wanapodharauliwa, wanaposhitakiwa na kutuhumiwa kwa uwongo na zaidi wanaposahauliwa, ili Kristo Yesu aweze kupewa sifa na utukufu zaidi!

Papa Leo XIV Mabalozi wa Vatican
10 Juni 2025, 15:37