Serikali ya Hispania Yamkaribisha Papa Leo XIV Kutembelea Hispania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 11 Juni 2025 majira ya jioni, alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Pedro Sánchez Pérez-Castejón wa Hispania na ametumia fursa hii kumshukuru Mfalme Filippo wa VI na Malkia Letizia waliohudhuria kwenye Ibada ya Misa Takatifu, mwanzo wa huduma yake kwa Kanisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Dominika tarehe 18 Mei 2025. Katika mazungumzo yao kwa njia ya simu, wamejikita katika mada zenye mvuto na mashiko kwa pande zote mbili, hususan: wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia; umuhimu wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu ili kujenga dunia katika misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano, ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Baba Mtakatifu Leo XIV pamoja na Rais wa Hispania wamezungumzia kuhusu Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo Fungamani ya binadamu (The Fourth International Conference on Financing for Development (FfD4) utakaofanyika kuanzia tarehe 30 Juni hadi tarehe 3 Julai 2025, huko Seville, nchini Hispania. Mkutano huu ni wakati muhimu wa kushughulikia changamoto za haraka za ufadhili na kusaidia kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu. Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo Fungamani ya binadamu (FfD4) unalenga pamoja na mambo mengine: kufungua mtaji zaidi, kurekebisha usanifu wa fedha Kimataifa, kuimarisha ushirikiano na mafungamano ya Kimataifa hasa kwa nchi zinazoendelea duniani. Rais Pedro Sánchez Pérez-Castejón wa Hispania ametumia fursa hii, kumwalika Baba Mtakatifu Leo XIV kutembelea nchini Hispania.